Jumatatu, 16 Machi 2015

Ongezeko la picha za watoto mitandaoni siyo sahihi

Maendeleo ni matokeo ya jitihada na nguvu zilizotumika katika kuwekeza. Taifa haliwezi kupata maendeleo ya kweli mpaka pale thamani ya watoto wake inapowekwa wazi kwa kila raia.

Mtoto ni rasilimali ambayo ikiandaliwa vyema taifa linaweza kufikia maendeleo na kuondokana na umasikini. Familia, jamii na taifa kwa ujumla tuna wajibu wa kutambua thamani ya watoto, kuwathamini, kuwalinda na kuwapatia haki zao kama elimu. Kufanya hivyo kutakuza vipaji vyao ambavyo baadaye vitakua taaluma.

Jinsi utandawazi unavyozidi kuenea, tumekuwa tukizidi kuona picha za watato wadogo mitandaoni wakiwa watupu bila nguo, wengine wameshika chupa za pombe kana kwamba wanakunywa na wengine wakivuta sigara.Je, hizi picha zinawapa watoto ujumbe gani?

Kama mtoto akifanya kosa mzazi unampiga picha badala ya kumuelekeza, unamfundisha nini? Inakera sana kuona ongezeko la usambazaji wa picha na video za watoto wadogo wakiwa uchi wakifanya ngono.

Jamii itambue kuwa ni kosa la jinai kisheria kurekodi mtoto katika hali yoyote bila idhini ya mzazi au mlezi wake. Vilevile ni kosa la kimaadili na kitaaluma (kwa mpiga picha) kuweka video ya mtoto akiwa mtupu bila kuficha sura yake kwa ajili ya kumlinda mtoto huyu. Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inatamka wazi kwamba ‘Mtu hatachapisha, kutengeneza, kuonyesha au kuagiza kuchapishwa, kuendeshwa au kuonyeshwa picha au taswira ya mtoto au mtoto aliyefariki, inayoonyesha ukatili au katika pozi za ngono.’ Sheria inatamka kwamba yeyote atakayekiuka masharti ya maelekezo ya kutopiga ama kuchapisha picha za mtoto kama ilivyoelezwa hapo juu, anatenda kosa la jinai na atakapotiwa hatiani atalipa faini isiyopungua shilingi laki tano au kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja. Ama kwa kujua au kutokujua, jamii hukiuka sheria hii mara nyingi.

Picha hizi hudhalilisha watoto, familia zao na hata kuwaathiri kisaikolojia watoto wenyewe na rafiki zao ambao pia ni watoto.

Haziwasaidii kwa namna yeyote zaidi ya kuharibu heshima na utu wa watoto hawa na kudhoofisha ukuaji na maendeleo yao. Watoto ni kama vioo, wanaakisi kile wanachokiona mbele yao. Wahalifu katika kupiga na kusambaza picha za watoto mitandaoni ni jamii nzima hasa wanaochekelea wakipata picha hizi na wenye mshawawa wa kuzisambaza kwenye makundi yao mitandaoni. Wengine ni wamiliki wa vibanda vya filamu mtaani, maarufu kama ‘vibanda umiza’. Hawa wanaonyesha filamu za aina zote bila kujali umri wa wateja wao. Watoto wadogo wanaruhusiwa kuingia kuona filamu za ngono alimuradi wanazo pesa za kiingilio. Ingawa mzazi huwezi kuwa kila mahala alipo mwanao. Kama jamii na taifa kwa ujumla tunao wajibu wa kuhakikisha tunawakinga watoto na mambo yanayoweza kuhafifisha ukuaji wa vipaji vyao na maendeleo yao.

Ili tuweze kuwekeza kupitia watoto hawana budi kuheshimiwa utu wao. Ni jukumu la jamii nzima kuepuka kusambaza picha za watoto zinazodhalilisha utu wao, jambo ambalo limeenea sana hasa katika mitandao ya kijamii. Kufanya hivyo kunaweza waathiri kisaikolojia, jambo linalodumaza maendeleo yao hata wanapokua watu wazima. Kama jamii na taifa kwa ujumla hatuna budi kuwawekea mazingira mazuri watoto yatakayo imarisha afya zao kimwili na kiakili ili kuandaa taifa la kizalendo litakalowajibika kikamilifu kukua kimaendeleo toka ngazi ya kaya hadi taifa. Wote kwa pamoja hatuna budi kuwapongeza pale wanapofanya vizuri, kuwatia moyo pale wanapokata tamaa kufanya jambo fulani na kuwaelekeza kwa upendo pale wanapokosea na si kuwapiga picha na kuchekelea makosa yao na rafiki zetu.

Makala haya yameandaliwa na wataalamu wa makuzi toka Sema

Source:http://www.mwananchi.co.tz

Jumanne, 10 Machi 2015

TEKNOLOJIA YA KISASA YA UKUSANYAJI WA TAARIFA KUTOKA KAMPUNI YA PUSH OBSERVER

Push Observer Limited ni kampuni ya Tanzania inayomiliki vyombo vya kiinteligencia na teknolojia ya sanaa ya kufuatilia, kukamata na kuchuja vyombo vya habari -magazeti, matangazo (radio & televisheni), Internet na uchambuzi, ripoti ya ushindani kwa ajili ya biashara, serikali na wateja wengineo wa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Hivi sasa, Push Observer wanachunguza vituo vya redio 90+, vituo vya televisheni 15+, magazeti (magazeti, majarida, magazeti na majarida) 70+ na machapisho online ikiwa ni pamoja na blogs na mitandao maudhui.

Observer ni kampuni ya kiTanzania inayoongoza kidigitali, kwa viwango vya kimataifa na ushirikiano wa kimataifa katika data na uanachama na vyombo kama FIBEP, Nudge, Vision Critical, na Harvard Innovation Labs. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mikakati wa Six Telecoms, Kampuni mama ya Push Observer, Rashid Shamte alisema kuwa kupitia teknologia hii ya usambazaji ya kisasa, wateja wao wataweza kupata habari taarifa muhimu na mpya masaa ishirini na nne ya wiki.

Aliongeza kuwa,tumezindua teknolojia hii kwa wateja wetu kutokana na teknologia ya uchunguzi wa vyombo vya habari kubadilika sana miaka ya karibuni”. “Huduma hii ya kusambaza taarifa imekuwa ya kisasa, rahisi na ya ubora wa hali ya juu kutokana na uwekezaji wetu katika teknolojia hii. Wana vifaa vya kisasa ambavyo vinaweza kupata taarifa kupitia televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na redio kwa muda muafaka, vifaa hivyo vinauwezo wa kupata taarifa had 350,000 kutoka vyombo mbali mbali. Kwa kutambua mahitaji ya wateja wetu kupata habari na taarifa za muhimu tumeamua kuzindua huduma hii na ili kuwahakikishia wateja wetu upatikanaji wa taarifa muhimu na taarifa zinginezo za kwene vyombo vya habari kwa muda muafaka” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Push Observer, Tom Kyalo.

Jumatano, 4 Machi 2015

Jenga uadilifu kwa kupinga rushwa

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kujenga uadilifu kwa kila mtu katika nchi yake, ni kukataa rushwa kwa kutoa au kupokea.

Sefue aliyasema hayo katika Warsha ya Wadau ya kujadili Rasimu ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi,Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi iliyoandaliwa na Tume ya Maadili iliyofanyika leo katika ukumbi wa Hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam,alisema wazo la ahadi ya Uadilifu kwa viongozi,watumishi wa Umma na sekta binafsi ni mwanzo wa kampeni kwa nchi nzima.

Alisema sheria kali na adhabu,lakini iwe ni dhamira ya kila mmoja kufuata maadili na kujenga utamaduni wa kutotoa rushwa au kupokea rushwa. Sefue alisema ahadi hizo zitatumika kama muongozo kwa kuzingatia makampuni yaliyotia saini pamoja na viongozi na watumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao, hivyo kutachangia katika juhudi za kupambana na rushwa nchini.

Aidha alisema lengo la 3.2 la dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 inayohusu Uongozi bora na utawala wa sheria inakusudia Tanzania kuwa jamii yenye maadili mema ,kuthamini ,utamaduni ,uadilifu,kuheshimu utawala wa sheria na kutokuwepo kwa rushwa na maovu.

Kwa upande wake Kamishina wa Tume ya Maadili, Jaji Mstaafu,Salome Kaganda, alisema rasimu ya ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi,Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi ni juhudi za kuunga mkono zilizopo za kukuza uadilifu uwazi na uwajibikaji katika kuimarisha utawala bora nchini.

Salome alisema kuwa walikuwa wakiangaliwa ni watumishi wa umma sasa watahusika sekta binafsi,wanasiasa na wafanyabiashara katika kujenga utawala bora katika nchi.

Source:MICHUZI BLOG

Jumapili, 1 Machi 2015

FAHAMU UMUHIMU WA SAIKOLOJIA YA ELIMU

Unaweza kuwa umeshawahi kusikia neno SAIKOLOJIA mara nyingi sana, Lakini hebu tufafanue zaidi kwa yule ambaye hafahamu maana yake.

Kwa kifupi kwanza hili neno ambalo asili yake ni kigiriki likiwa na maana ya kwamba, saiko ni mambo yanayohusu akili au ubongo, na lojia ni mambo yanayohusu elimu.

Hivyo kwa ujumla tunaweza kusema kwamba saikolojia ni elimu inayohusu mambo ya akili au ubongo. Somo hili la saikolojia linahusu jinsi wanyama na binadamu wanavyoweza kutumia akili au ubongo katika kumiliki na kuongoza vitendo na tabia zao. Ni wazi kuwa wanyama wote wana ubongo Lakini ni binadamu peke yake ndiye mwenye uwezo wa kujifunza kwa kutumia ubongo wake wakati wanyama wengine hujifunza kwa kutumia silika na mazoea. Na hii humfanya binadamu kuwa tofauti na viumbe wengine.

Sehemu kubwa ya saikolojia inahusu jinsi binadamu anavyoweza kutumia ubongo au akili yake katika kujifunza, kufikiri na kudhibiti tabia zake. Kwa ujumla ni kwamba saikolojia ni taaluma ya kisayansi inayohusu tabia/mienendo na michakato ya ubongo au akili ya binadamu katika kujifunza. Tabia au mienendo ni kila kitu ambacho mtu hufanya na ambacho huweza kuchunguzwa moja kwa moja.

Tumeangalia kwa ufupi sana maana halisi ya saikolojia, sasa je unaelewa nini kuhusu saikolojia ya elimu? Kuna matawi mbalimbali ya saikolojia kama vile saikolojia ya Elimu, Saikolojia ya Kliniki, saikolojia ya Biashara, saikolojia ya Kijeshi n.k. hivyo basi katika mada hii tunaangalia maana ya saikolojia ya elimu na umuhimu wake.

Saikolojia ya elimu ni tawi la taaluma ya saikolojia linaloshughulikia masuala ya elimu, tawi hili linachunguza jinsi mwanafunzi anavyojifunza mambo mbalimbali ya kielimu, kijamii na kiutamaduni na namna bora ya kumfundisha. Sasa hebu tuangalie tawi hili lina umuhimu gani? Au kuna umuhimu gani wa mwalimu kujua saikolojia?

Umuhimu wa saikolojia ya Elimu

1. Hii humsaidia mwalimu kujua tabia za mwanafunzi na kujua ni kwa njia au mbinu gani anaweza kuzitumia ili tendo la kujifunza litokee na pia kujua sababu zinazoweza kufanya tendo la kujifunza lisiimarike mfano wanafunzi hutofautiana sana kutokana na malezi waliyolelewa au mahala walipotokea, hivyo kama mwalimu ukishajua tofauti hizi utajua utumie mbinu zipi ili kuhakikisha kuna usawa wa elimu au ulichokifundisha kimeeleweka kwa wote bila ya kubagua mwenye uwezo mkubwa au mdogo.

2. Husadia pia kujua jinsi ubongo au akili ya binadamu inavyotumika katika tendo la kujifunza. Kujua huku kutafufua njia na mbinu mbalimbali kuhakikisha kinachofundishwa kimefanikiwa.

3. Husaidia kumjua vema mwanafunzi wako na kujua jinsi gani utamsaidia ili ajifunze vema zaidi.

4. Itakusaidia kufahamu matatizo yanayokwamisha mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji na kujua jinsi gani utaweza kuyatatua.

5. Kwa kufahamu saikolojia na tabia za wanafunzi wako utaweza kuwaandaa vema na kuwapa motisha ili walipende somo na kuwachochea inapobidi. Mfano unaweza kutumia mifano mizuri ya kile wanafunzi wanachokipenda ili kuwafanya wawe na furaha na umakini na kile unachokifundisha.

6. Utajua kama mwanafunzi ameelewa au hajakuelewa hata kama amekaa kimya bila ya kukuuliza au kusema lolote. Kuna wanafunzi huwa na uoga wa kuuliza swali pale anaposhindwa kuelewa sehemu fulani, hivyo kama una ujuzi wa saikolojia hali hii unaweza kuigundua kwa wanafunzi wako na kuirekebisha.

Kwa upande wangu nina hayo machache, ikiwa una lolote la kuongezea jisikie huru kuacha maoni yako kwani tuko pamoja katika kuelimisha jamii katika mambo mbalimbali.

Kwa maoni wasiliana nami,
CHACHA,J.Clement
Librarian-Chuo kikuu cha Dodoma
Email:jacksonclement73@gmail.com