Maendeleo ni matokeo ya jitihada na nguvu zilizotumika katika kuwekeza. Taifa haliwezi kupata maendeleo ya kweli mpaka pale thamani ya watoto wake inapowekwa wazi kwa kila raia.
Mtoto ni rasilimali ambayo ikiandaliwa vyema taifa linaweza kufikia maendeleo na kuondokana na umasikini. Familia, jamii na taifa kwa ujumla tuna wajibu wa kutambua thamani ya watoto, kuwathamini, kuwalinda na kuwapatia haki zao kama elimu. Kufanya hivyo kutakuza vipaji vyao ambavyo baadaye vitakua taaluma.
Jinsi utandawazi unavyozidi kuenea, tumekuwa tukizidi kuona picha za watato wadogo mitandaoni wakiwa watupu bila nguo, wengine wameshika chupa za pombe kana kwamba wanakunywa na wengine wakivuta sigara.Je, hizi picha zinawapa watoto ujumbe gani?
Kama mtoto akifanya kosa mzazi unampiga picha badala ya kumuelekeza, unamfundisha nini? Inakera sana kuona ongezeko la usambazaji wa picha na video za watoto wadogo wakiwa uchi wakifanya ngono.
Jamii itambue kuwa ni kosa la jinai kisheria kurekodi mtoto katika hali yoyote bila idhini ya mzazi au mlezi wake. Vilevile ni kosa la kimaadili na kitaaluma (kwa mpiga picha) kuweka video ya mtoto akiwa mtupu bila kuficha sura yake kwa ajili ya kumlinda mtoto huyu. Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inatamka wazi kwamba ‘Mtu hatachapisha, kutengeneza, kuonyesha au kuagiza kuchapishwa, kuendeshwa au kuonyeshwa picha au taswira ya mtoto au mtoto aliyefariki, inayoonyesha ukatili au katika pozi za ngono.’ Sheria inatamka kwamba yeyote atakayekiuka masharti ya maelekezo ya kutopiga ama kuchapisha picha za mtoto kama ilivyoelezwa hapo juu, anatenda kosa la jinai na atakapotiwa hatiani atalipa faini isiyopungua shilingi laki tano au kifungo cha miezi sita au vyote kwa pamoja. Ama kwa kujua au kutokujua, jamii hukiuka sheria hii mara nyingi.
Picha hizi hudhalilisha watoto, familia zao na hata kuwaathiri kisaikolojia watoto wenyewe na rafiki zao ambao pia ni watoto.
Haziwasaidii kwa namna yeyote zaidi ya kuharibu heshima na utu wa watoto hawa na kudhoofisha ukuaji na maendeleo yao. Watoto ni kama vioo, wanaakisi kile wanachokiona mbele yao. Wahalifu katika kupiga na kusambaza picha za watoto mitandaoni ni jamii nzima hasa wanaochekelea wakipata picha hizi na wenye mshawawa wa kuzisambaza kwenye makundi yao mitandaoni. Wengine ni wamiliki wa vibanda vya filamu mtaani, maarufu kama ‘vibanda umiza’. Hawa wanaonyesha filamu za aina zote bila kujali umri wa wateja wao. Watoto wadogo wanaruhusiwa kuingia kuona filamu za ngono alimuradi wanazo pesa za kiingilio. Ingawa mzazi huwezi kuwa kila mahala alipo mwanao. Kama jamii na taifa kwa ujumla tunao wajibu wa kuhakikisha tunawakinga watoto na mambo yanayoweza kuhafifisha ukuaji wa vipaji vyao na maendeleo yao.
Ili tuweze kuwekeza kupitia watoto hawana budi kuheshimiwa utu wao. Ni jukumu la jamii nzima kuepuka kusambaza picha za watoto zinazodhalilisha utu wao, jambo ambalo limeenea sana hasa katika mitandao ya kijamii. Kufanya hivyo kunaweza waathiri kisaikolojia, jambo linalodumaza maendeleo yao hata wanapokua watu wazima. Kama jamii na taifa kwa ujumla hatuna budi kuwawekea mazingira mazuri watoto yatakayo imarisha afya zao kimwili na kiakili ili kuandaa taifa la kizalendo litakalowajibika kikamilifu kukua kimaendeleo toka ngazi ya kaya hadi taifa. Wote kwa pamoja hatuna budi kuwapongeza pale wanapofanya vizuri, kuwatia moyo pale wanapokata tamaa kufanya jambo fulani na kuwaelekeza kwa upendo pale wanapokosea na si kuwapiga picha na kuchekelea makosa yao na rafiki zetu.
Makala haya yameandaliwa na wataalamu wa makuzi toka Sema
Source:http://www.mwananchi.co.tz