Jumatano, 4 Machi 2015

Jenga uadilifu kwa kupinga rushwa

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kujenga uadilifu kwa kila mtu katika nchi yake, ni kukataa rushwa kwa kutoa au kupokea.

Sefue aliyasema hayo katika Warsha ya Wadau ya kujadili Rasimu ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi,Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi iliyoandaliwa na Tume ya Maadili iliyofanyika leo katika ukumbi wa Hoteli ya New Afrika jijini Dar es Salaam,alisema wazo la ahadi ya Uadilifu kwa viongozi,watumishi wa Umma na sekta binafsi ni mwanzo wa kampeni kwa nchi nzima.

Alisema sheria kali na adhabu,lakini iwe ni dhamira ya kila mmoja kufuata maadili na kujenga utamaduni wa kutotoa rushwa au kupokea rushwa. Sefue alisema ahadi hizo zitatumika kama muongozo kwa kuzingatia makampuni yaliyotia saini pamoja na viongozi na watumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao, hivyo kutachangia katika juhudi za kupambana na rushwa nchini.

Aidha alisema lengo la 3.2 la dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 inayohusu Uongozi bora na utawala wa sheria inakusudia Tanzania kuwa jamii yenye maadili mema ,kuthamini ,utamaduni ,uadilifu,kuheshimu utawala wa sheria na kutokuwepo kwa rushwa na maovu.

Kwa upande wake Kamishina wa Tume ya Maadili, Jaji Mstaafu,Salome Kaganda, alisema rasimu ya ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi,Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi ni juhudi za kuunga mkono zilizopo za kukuza uadilifu uwazi na uwajibikaji katika kuimarisha utawala bora nchini.

Salome alisema kuwa walikuwa wakiangaliwa ni watumishi wa umma sasa watahusika sekta binafsi,wanasiasa na wafanyabiashara katika kujenga utawala bora katika nchi.

Source:MICHUZI BLOG

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni